Friday, February 14, 2020

VITU KUMI HATARI KWA AJILI YA SAUTI YAKO.


An ink wood engraving from 1875 - showing the anatomy of a human larynx


Nakushukuru ndugu msomaji wangu kwa kuendelea kufuatilia makala hizi. 

Nilikuwa naongea na Tabibu kutoka Hospitali ya wilaya ya Chato, Paul. M.Kahindi kuhusu jinsi ya kutunza sauti zetu na madhara yanayoweza kutokea na kuharibu sauti zetu baada ya kutumia baadhi ya vitu, tabia ama matibabu. Namshukuru sana huyu tabibu na Mungu ambariki sana na aendelee kummiminia neema na baraka zake katika kazi zake.

Kuimba, kuongea nakutumia sauti kwa mambo mbalimbali ni kipaji na ni wito. Mungu ndiye anayegawa kipaji hiki lakini kila mmoja anaweza kuimba ilimradi tu anajua kuongea, ukijifunza au kufundishwa vizuri jinsi ya kuimba. 

Swali ni kwamba; Unaweza kuwa mtu ambaye unaongea sana, muimbaji au mcheshi lakini ni kwa kiasi gani unaifahamu sauti yako hiyo ambayo ni nzuri na inayofurahisha na kustastaajabisha, ukilipata jibu hapa basi unaweza kuungana na mimi katika harakati za kuitengeneza sauti yako iweze kudumu katika ubora wake.

Watoto huwa wanaakisi lafudhi za wazazi wao wakati wakiwa bado tumboni
Watafiti waliwachunguza watoto waliozaliwa Ufaransa na Ujerumani na kubaini kuwa kile kilio ambacho huwa wanakitoa wakati wanazaliwa huwa ndio lugha ya mama zao na wameonyesha pia namna ambavyo inawezekana kujua watoto hawa wametoka mataifa tofauti kwa namna ambavyo wanalia

Sauti huwa inajihifadhi katika sehemu maalum ndani ya mwili wako. Sauti yako inaanzia kutoka ndani, ukiwa unahema taratibu huwa inaendeshwa na sanduku linalohifadhi sauti (voice box), Vipande viwili vya tishu hutikisika kwa kwenda mbele na kurudi nyuma wakati ambapo hewa inapita mdundo wa sauti unatengenezwa.

Kama wewe ni Mwanakwaya, mwimbaji, msanii au mshereheshaji  au ni mtu unayehitaji kutumia sauti yako kuongea na kundi fulani la watu, kuimba au kwa chochote, nakushauri utunze sana sauti yako kwa kuzingatia mambo muhimu kwa ajili ya kutunza sauti na kuifanya idumu kwa ubora mpaka Mungu atakapokuita kutoka hapa duniani. Kwa maana hiyo, ni lazima kwa makundi ya watu niliyoyasema hapo juu kuwa makini na vyakula, vinywaji na mfumo wa maisha tunayoishi ili kuepuka tatizo la kuharibu sauti yakomaana sauti hii tunayoiongelea leo inaweza kukupatia pesa na faida zingine kwako binafsi,  kwa Mungu, kwa jamii na kwa serikali pia. (Tumia sauti yako kama mtaji wako!)


 VITU KUMI HATARI KWA SAUTI YAKO


Kuna vitu vingi sana vinavyoweza kuharibu sauti yako ewe msanii wa sauti (mwanakwaya, mwimbaji, msanii na mtoa hotuba) lakini kwa leo nitakuelezea vitu kumi. 

Kama nilivyokueleza hapo juu kuhusu jinsi inavyotengenezwa sauti na umuhimu wa kuitunza sauti yako, unatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo ili sauti yako iwe vizuri na kwenye ubora usioharibika;

  1. POMBE.  Pombe ni kinyaji kizuri sana kwa ajiri ya kuburudisha akili na ubongo wa mwanadamu kwa ujumla, lakini ina madhara makubwa sana kwa afya ya msanii, mwanakwaya, mshereheshaji na watu wengine wanaotumia sauti zao kuongea na jamii kwa njia yoyote ile.Pombe huongeza saizi na kubadilisha muonekano wa mapafu na mfumo wa sauti kwa ujumla. kwa maana hiyo, pombe huharibu sauti ya mwimbaji au mfikisha taarifa/ujumbe kwa njia ya sauti kwa kuharibu mfumo wa utendaji kazi wa mapafu. lakini pia pombe huchoma koo kwa kilevi kilichomo na baadae husababisha kansa ya koo. (Hii ni hatari sana kwa mwimbaji na kwa jamii pia)  (ILI KUTUNZA SAUTI YAKO, ACHA KABISA KUNYWA POMBE.)

  1. Matumizi ya dawa kwa muda mrefu. Sote tunajua kuwa, ili sauti iwe vizuri, unatakiwa kuwa na afya njema sana kila wakati. Dawa ni sumu na ina tindikali pia (kwa baadhi ya dawa) na   inaweza kuharibu chochote katika mfumo wa afya ya mwanadamu. Matumizi ya dawa ya muda mrefu husababisha kuuawa kwa kinga mama za mwili (self immunit) Mfano. Matumizi ya Chrolomphenicol kwa muda mrefu husababisha madonda mdomoni na hii inaweza kusababisha upweke na kujitenga kwenye kundi la watu au kushindwa kutimiza jukumu lako kwa wakati muafaka)  


  1. Matumizi ya sigara: Kama nilivyokueleza hapo juu, sigara pia ina tindikali (Nicotin) ambayo huingia katika mfumo wa hewa (trachea, mapafu , Vocal cord) na husababisha ukungu katika mapafu na mfumo wa sauti kwa ujumla. Lakini pia,  ukungu husababisha msukumo wa damu kuwa mkubwa zaidi na kusababisha kupasuka kwa mishipa inayosafirisha damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye mapafu, hii hali ikitokea husababisha hata mtu kutapika damu kwa kuwa mshipa huo umeshapasuka. Hii hutokea pia hata kwa wananokunywa pombe sana na wanaotumia madawa mbalimbali ya kulevya.

  1. Matibabu ya upasuaji wa koo. Hii pia ni tatizo kwa waimbaji japo siombei mtu kufanyiwa upasuaji. Mtu aliyefanyiwa upasuaji wa koo ana shida katika utoaji wa sauti. Mtu huyu kama yupo kwenye kikundi fulani, anatakiwa kupewa ruhusa kwenye baadhi ya mazoezi katika uimbaji.


  1. Ulaji wa vyakula vya baridi sana, vya moto sana au vyenye tindikali kama limao n.k., Ulaji wa vyakula hivi husababisha madhara kwa msanii, mwimbaji, msemaji  kwa sababu, vyakula vya baridi hubadilisha hata mfumo wa sauti. Vyakula vya moto huchoma  koo na kusababisha kuuawa kwa baadhi ya seli za mwili na hivyo kuharibu mfumo mzima wa sauti.

  1. Maambukizi katika njia ya koo. (KOO NDILO MTAJI KATIKA SAUTI), na kama tunatambua hilo,tumeshajua umuhimu wa koo katika kazi hii ya kuwasiliana na jamii kwa njia mbalimbali kama za nyimbo, kwaya, kuongea n.k


  1. Ugonjwa wa koo; Watu wenye magonjwa ya koo wanapata shida sana katika kuimba au  kuongea na hadhira. sitawaongelea sana hawa watu kwa siku ya leo, lakini pia, ugonjwa huu huathiri sauti kwa kiwango kikubwa.

  1. Matibabu ya mionzi kwenye koo; Nakuomba ndugu yangu ambaye kipaji chako ni kufikisha ujumbe wako kwa hadhira kwa njia ya sauti, usipende sana matibabu haya japo yakihitajika ni lazima ufanyiwe tu. Matibabu haya husababisha sauti kubadilika kutoka kwenye uhalisia.


  1. Kurithi; Kuna matatizo mengine ya kurithi yanayoweza kusababisha sauti yako kuwa mbaya, matatizo haya yanaweza kuwa ya kiakii, kisaikolojia n.k. Mtoto huwa anarithi sauti ya mzazi wake tangu akiwa tumboni na hata akizaliwa, sauti anayoitoa wakati analia ni uhalisia wa sauti ya mama yake. Kwa maana hiyo, mtoto huyu anaweza kurithi sauti kutoka kwa mzazi wake.

  1. Kupiga kelele na kufanya kazi zinazoambatana na kupiga kelele; Kuna baadhi ya sekta za kiserikari na binafsi huwa na utaratibu wa kupiga kelele mara kwa mara kama jeshini, (mf. Mguuuuuuu pandeee!), wapiga debe stendi n.k Watu hawa huishi kwa sauti hizo walizozizoea, kwa hiyo kama atakuwa ni msanii ataitumia sauti yake kwenye kipaji chake na wakati mwingine atatumia hata kwenye maongezi. Hili nadhani kila mtu analijua na tunaliona katika jamii inayotuzunguka.


Hayo ndiyo mambo niliyokuandalia leo lakini tujue kuwa uongeaji wetu, Uimbaji wetu na kipaji chetu kinatakiwa kuakisi yale tunayoyaishi. 




Imeandikwa na; 
Emmanuel W Shimbala
Katibu
SEM BAND TANZANIA
CHATO-GEITA TANZANIA
+255 762 176 662 au +255 756 446 979
E-mail: sembandtanzania@gmail.com


No comments:

VITU KUMI HATARI KWA AJILI YA SAUTI YAKO.

Nakushukuru ndugu msomaji wangu kwa kuendelea kufuatilia makala hizi.  Nilikuwa naongea na  Tabibu kutoka Hospitali ya wilaya ya C...