Nakushukuru ndugu msomaji wangu kwa kuendelea kufuatilia makala hizi.
Nilikuwa naongea na Tabibu kutoka Hospitali ya wilaya ya Chato, Paul. M.Kahindi kuhusu jinsi ya kutunza sauti zetu na madhara yanayoweza kutokea na kuharibu sauti zetu baada ya kutumia baadhi ya vitu, tabia ama matibabu. Namshukuru sana huyu tabibu na Mungu ambariki sana na aendelee kummiminia neema na baraka zake katika kazi zake.
Kuimba, kuongea nakutumia sauti kwa mambo mbalimbali ni kipaji na ni wito. Mungu ndiye anayegawa kipaji hiki
lakini kila mmoja anaweza kuimba ilimradi tu anajua kuongea, ukijifunza au
kufundishwa vizuri jinsi ya kuimba.
Swali ni kwamba; Unaweza
kuwa mtu ambaye unaongea sana, muimbaji au mcheshi lakini ni kwa kiasi gani
unaifahamu sauti yako hiyo ambayo ni nzuri na inayofurahisha na
kustastaajabisha, ukilipata jibu hapa basi unaweza kuungana na mimi katika
harakati za kuitengeneza sauti yako iweze kudumu katika ubora wake.
Watoto
huwa wanaakisi lafudhi za wazazi wao wakati wakiwa bado tumboni
Watafiti
waliwachunguza watoto waliozaliwa Ufaransa na Ujerumani na kubaini kuwa kile
kilio ambacho huwa wanakitoa wakati wanazaliwa huwa ndio lugha ya mama zao na wameonyesha
pia namna ambavyo inawezekana kujua watoto hawa wametoka mataifa tofauti kwa
namna ambavyo wanalia
Sauti
huwa inajihifadhi katika sehemu maalum ndani ya mwili wako. Sauti
yako inaanzia kutoka ndani, ukiwa unahema taratibu huwa inaendeshwa na sanduku
linalohifadhi sauti (voice box), Vipande viwili vya tishu hutikisika kwa
kwenda mbele na kurudi nyuma wakati ambapo hewa inapita mdundo wa sauti
unatengenezwa.
Kama wewe ni Mwanakwaya, mwimbaji, msanii au
mshereheshaji au ni mtu unayehitaji kutumia sauti yako kuongea na kundi
fulani la watu, kuimba au kwa chochote, nakushauri utunze sana sauti
yako kwa kuzingatia mambo muhimu kwa ajili ya kutunza sauti na kuifanya idumu
kwa ubora mpaka Mungu atakapokuita kutoka hapa duniani. Kwa maana hiyo, ni
lazima kwa makundi ya watu niliyoyasema hapo juu kuwa makini na vyakula,
vinywaji na mfumo wa maisha tunayoishi ili kuepuka tatizo la kuharibu sauti
yakomaana sauti hii tunayoiongelea leo inaweza kukupatia pesa na faida zingine
kwako binafsi, kwa Mungu, kwa jamii na kwa serikali pia. (Tumia
sauti yako kama mtaji wako!)
Kuna vitu vingi sana vinavyoweza kuharibu sauti yako ewe msanii wa
sauti (mwanakwaya, mwimbaji, msanii na mtoa hotuba) lakini kwa leo nitakuelezea vitu kumi.
Kama nilivyokueleza hapo
juu kuhusu jinsi inavyotengenezwa sauti na umuhimu wa kuitunza sauti yako,
unatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo ili sauti yako iwe vizuri na kwenye ubora
usioharibika;
- POMBE. Pombe
ni kinyaji kizuri sana kwa ajiri ya kuburudisha akili na ubongo wa
mwanadamu kwa ujumla, lakini ina madhara makubwa sana kwa afya ya msanii,
mwanakwaya, mshereheshaji na watu wengine wanaotumia sauti zao kuongea na
jamii kwa njia yoyote ile.Pombe huongeza saizi na kubadilisha muonekano wa
mapafu na mfumo wa sauti kwa ujumla. kwa maana hiyo, pombe huharibu sauti
ya mwimbaji au mfikisha taarifa/ujumbe kwa njia ya sauti kwa kuharibu mfumo
wa utendaji kazi wa mapafu. lakini pia pombe huchoma koo kwa kilevi
kilichomo na baadae husababisha kansa ya koo. (Hii ni hatari sana kwa
mwimbaji na kwa jamii pia) (ILI KUTUNZA SAUTI YAKO, ACHA KABISA KUNYWA POMBE.)
- Matumizi
ya dawa kwa muda mrefu. Sote tunajua kuwa, ili sauti iwe vizuri, unatakiwa
kuwa na afya njema sana kila wakati. Dawa ni sumu na ina tindikali pia
(kwa baadhi ya dawa) na inaweza kuharibu chochote katika mfumo
wa afya ya mwanadamu. Matumizi ya dawa ya muda mrefu husababisha kuuawa kwa
kinga mama za mwili (self immunit) Mfano. Matumizi ya Chrolomphenicol kwa
muda mrefu husababisha madonda mdomoni na hii inaweza kusababisha upweke
na kujitenga kwenye kundi la watu au kushindwa kutimiza jukumu lako kwa
wakati muafaka)
- Matumizi
ya sigara: Kama nilivyokueleza hapo juu, sigara pia ina tindikali
(Nicotin) ambayo huingia katika mfumo wa hewa (trachea, mapafu , Vocal
cord) na husababisha ukungu katika mapafu na mfumo wa sauti kwa ujumla.
Lakini pia, ukungu husababisha msukumo wa damu kuwa mkubwa zaidi na
kusababisha kupasuka kwa mishipa inayosafirisha damu kutoka kwenye moyo
kwenda kwenye mapafu, hii hali ikitokea husababisha hata mtu kutapika damu
kwa kuwa mshipa huo umeshapasuka. Hii hutokea pia hata kwa wananokunywa
pombe sana na wanaotumia madawa mbalimbali ya kulevya.
- Matibabu
ya upasuaji wa koo. Hii pia ni tatizo kwa waimbaji japo siombei mtu
kufanyiwa upasuaji. Mtu aliyefanyiwa upasuaji wa koo ana shida katika
utoaji wa sauti. Mtu huyu kama yupo kwenye kikundi fulani, anatakiwa
kupewa ruhusa kwenye baadhi ya mazoezi katika uimbaji.
- Ulaji
wa vyakula vya baridi sana, vya moto sana au vyenye tindikali kama limao
n.k., Ulaji wa vyakula hivi husababisha madhara kwa msanii, mwimbaji,
msemaji kwa sababu, vyakula vya baridi hubadilisha hata mfumo wa sauti.
Vyakula vya moto huchoma koo na kusababisha kuuawa kwa baadhi ya
seli za mwili na hivyo kuharibu mfumo mzima wa sauti.
- Maambukizi
katika njia ya koo. (KOO NDILO MTAJI KATIKA SAUTI), na kama tunatambua
hilo,tumeshajua umuhimu wa koo katika kazi hii ya kuwasiliana na jamii kwa
njia mbalimbali kama za nyimbo, kwaya, kuongea n.k
- Ugonjwa
wa koo; Watu wenye magonjwa ya koo wanapata shida sana katika kuimba
au kuongea na hadhira. sitawaongelea sana hawa watu kwa siku ya leo, lakini pia, ugonjwa huu huathiri sauti kwa kiwango kikubwa.
- Matibabu
ya mionzi kwenye koo; Nakuomba ndugu yangu ambaye kipaji chako ni kufikisha ujumbe
wako kwa hadhira kwa njia ya sauti, usipende sana matibabu haya japo
yakihitajika ni lazima ufanyiwe tu. Matibabu haya husababisha sauti
kubadilika kutoka kwenye uhalisia.
- Kurithi;
Kuna matatizo mengine ya kurithi yanayoweza kusababisha sauti yako kuwa
mbaya, matatizo haya yanaweza kuwa ya kiakii, kisaikolojia n.k. Mtoto huwa anarithi sauti ya mzazi wake tangu akiwa tumboni na hata akizaliwa, sauti anayoitoa wakati analia ni uhalisia wa sauti ya mama yake. Kwa maana hiyo, mtoto huyu anaweza kurithi sauti kutoka kwa mzazi wake.
- Kupiga
kelele na kufanya kazi zinazoambatana na kupiga kelele; Kuna baadhi ya sekta za kiserikari na binafsi huwa na utaratibu wa
kupiga kelele mara kwa mara kama jeshini, (mf. Mguuuuuuu pandeee!), wapiga debe stendi n.k Watu hawa
huishi kwa sauti hizo walizozizoea, kwa hiyo kama atakuwa ni msanii ataitumia sauti yake kwenye kipaji chake na wakati mwingine atatumia hata
kwenye maongezi. Hili nadhani kila mtu analijua na tunaliona katika jamii inayotuzunguka.
Hayo ndiyo mambo niliyokuandalia leo lakini tujue kuwa uongeaji wetu, Uimbaji wetu na kipaji chetu kinatakiwa kuakisi yale
tunayoyaishi.
Imeandikwa na;
Emmanuel W Shimbala
Katibu
SEM BAND TANZANIA
CHATO-GEITA TANZANIA
+255 762 176 662 au
+255 756 446 979
E-mail:
sembandtanzania@gmail.com